IQNA

Muislamu afungwa jela miaka 16 China baada ya kupatikana na Audio za Qur'ani

10:15 - December 02, 2017
Habari ID: 3471291
TEHRAN (IQNA)-Muislamu mmoja nchini China amehukumiwa kifungo cha miaka 16 jela baada ya kupatikana na faili za sauti (Audio) za qiraa ya Qur'ani Tukufu kwenye kompyuta yake.

Taarifa zinasema mtu huyo kutoka kaumu ya Wakazakh amehukumiwa kifungo hicho kela katika eneo la Xinjiang lenye Waislamu wengi kusini magharibi mwa China.

Duru zinasema Manat Hamit mwenye umri wa miaka 45 awali alihukumiwa kifungo hicho Mei mwaka huu katika mahakama ya Kaunti ya Fuhai eneo la Xinjiang na rufaa yake ilikataliwa na mahakama ya juu.

Dada yake Manat, Nurisha Manat, ambaye anaishi katika nchi jirani ya Kazakhstan, anasema familia yake ilijaribu kumsaidia lakini wakuu wa eneo hilo wamekataa kutoa maelezo zaidi au kukubali wakili aliyekuwa amepanga kumtetea katika kesi ya rufaa.

Imedokewa kuwa Manat alikamatwa Aprili 25 baada ya maafisa wa serikali kupata faili kadhaa za sauti zilizokuwa na qiraa ya Qur'ani Tukufu katika kompyuta yake.

Muislamu huyo alikabiliwa na mashtaka ya kueneza ugaidi kupitia faili za sauti na kuchochea ubaguzi wa rangi huku familia yake ikilalamika kuwa alihukumiwa pasina kupewa fursa ya kuwa na wakili katika kesi yake.

Duru zinasema wakuu wa Uchina wamewakamata mamialia ya Waislamu mwezi huu na kufunga akaunti zao za benki au kuchukua udhibiti mali zao kwa kisingizio cha kuwachunguza kuhusu misimamo mikali ambayo inajumuisha kutekeleza ibada za kawaida za Kiislamu.

3464573

captcha