IQNA

Idadi ya Waislamu Russia ni Millioni 25

10:54 - March 08, 2018
Habari ID: 3471421
TEHRAN (IQNA)-Idadi ya Waislamu nchini Russia sasa imefika watu milioni 25 kati ya watu milioni 145 nchini humo, amesema Mufti Mkuu wa Russia Sheikh Rawil Gaynetdin.

Ameongeza kuwa, idadi ya Waislamu Russia inazidi kuongezeka kutokana na sababu mbili muhuimu, kwanza ni ongezeko la watoto wanaozaliwa katika familia za Waislamu na pili ni wahajiri kutoka eneo la Asia ya Kati. Amesema hata katika sensa ya serikali, idadi ya Waislamu pia imebainika kuongezeka.

Sheikh Gaynetdin amesema aghalabu ya Waislamu nchini Russia wanaishi katika mji mkuu Moscow na miji mingine mikubwa kama vile St. Petersburg and Yekaterinburg. Halikadhalika kuna idadi kubwa ya Waislamu katika majimbo yaliyokuwa ya Kiislamu kabla ya kuundwa shirikisho la Russia. Maeneo hayo ni pamoja na Tatarstan, Bashkortostan, na Jamhuri za Caucasus Kaskazini, amesema Mufti. Jamhuri za Caucasus au Kavkazia Kaskazini ni pamoja na Adygea, Chechnya, Dagestan, Ingushetia, Kabardino-Balkaria, Karachay-Cherkessia, Krasnodar Krai na Ossetia Kaskazini. Jamhuri zote hizo ziko katika Shirikisho la Russia lakini zenye mamlaka ya ndani ya kujitawala.

Halikadhalika Sheikh Gaynetdin amesema Waislamu ni wenyeji wa Russia ambapo zaidi ya kaumu 58 nchini humo zimekuwa za Waislamu tangu jadi.

Aidha amesema Uislamu uliwahi kutangazwa kuwa dini rasmi ya serikali katika moja ya majimbo ya Russia ya leo yaani, Volga Bulgaria, mnamo mwaka 922, miaka 66 kabla ya Ukristo wa Kiothodoxi kukubaliwa kama dini rasmi ya serikali katika utawala wa Kievan Rus.Idadi ya Waislamu Russia ni Millioni 25

Maelfu ya Waislamu katika Sala ya Idul Fitr katika Msikiti wa Jamia Moscow

"Uislamu uliingia Russia katika karne ya saba Miladia. Wafuasi wa Mtume Muhammad SAW waliwasili Russia miaka 22 baada ya mtukufu huyo kuaga dunia. Walikuja katika mji ambao sasa unajulikana kama Derbent, kusini mwa Daghestan. Adhana ya kwanza Russia ilikuwa katika ardhi ya Daghestan," amebainisha Mufti.

Aghalabu ya Waislamu wa Russia wanafuata madhehebu ya Hanafi lakini pia kuna Masunni wa Madhehebu ya Shafi na pia kuna Mashia, ameongeza Sheikh Gaynetdin.

3465339

captcha