IQNA

Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu kwa Munasaba wa Mwaka Mpya wa Hijria Shamsia

23:37 - March 20, 2018
Habari ID: 3471436
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei, ameutangaza mwaka mpya wa 1397 hijria shamsia kuwa mwaka wa "kuunga mkono bidhaa za Iran".

Katika ujumbe aliotoa kwa taifa usiku huu mara baada ya kuingia mwaka mpya wa 1397 hijria shamsia, Ayatullah Khamenei ametoa mkono wa heri na baraka kwa wananchi wote wa Iran, hususan familia azizi za mashahidi, majeruhi wa vita pamoja na chipukizi na vijana ambao ni tumaini la kusukuma mbele gurudumu la elimu nchini na kuwatakia wote sikukuu nzuri na ya furaha ya Nouruzi na mwaka mpya wenye wingi wa heri na baraka.

Katika tathimini aliyotoa kuhusu mipando na mishuko na matamu na machungu ya mwaka 1396, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, huo ulikuwa mwaka ulioshuhudia "kudhihiri kwa adhama, uwezo na kujitokeza kwenye medani wananchi wa Iran" na akaongezea kwa kusema: mwanzoni mwa mwaka, zaidi ya watu milioni 40 walishiriki kwa wingi na kwa namna ya kustaajabisha na yenye maana kubwa katika uchaguzi wa rais na wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji; na ushiriki huo uliendelea kushuhudiwa pia katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds, maandamano ya Dei 9 na ukashuhudiwa kwa ukubwa zaidi kwenye maandamano ya Bahman 22 ya maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Ayatullah Khamenei ameashiria pia mipango na njama zilizogonga mwamba za maadui za kutaka kuzusha machafuko katika miezi ya mwishoni mwa mwaka na kueleza kwamba maandamano yaliyofanywa na wananchi wenyewe kukabiliana na wazusha machafuko yameonyesha jinsi wananchi wa Iran wenye basira na uono mpana walivyojiweka tayari kujitokeza katika medani zote.

Ayatullah Khamenei aidha amesema, kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita, suala la msingi katika mwaka huu pia ni la uchumi na kushughulikia maisha ya wananchi na kusisitiza kwamba ikiwa uzalishaji wa kitaifa utafanyika kwa kasi na kwa hima na ufuatiliaji wa watu wote matatizo mengi ya maisha ya watu na masuala ya ajira na uwekezaji mitaji yatatatuka, na masaibu mengi ya kijamii yatapungua; na ni kwa msingi huo ameupa mwaka huu jina na kaulimbiu ya mwaka wa "kuunga mkono bidhaa za Iran".

Ayatullah Khamenei aidha amemsalia mtukufu Imam wa Zama Baqiyyatullah (Allah aharakishe kudhihiri kwake) na kuitakia rehma roho toharifu ya Imam Khomeini (MA) na kusisitiza kuwa kusadifiana machipuo ya maumbile na machipuo ya kimaanawi, yaani miezi ya Rajab, Shaaban na Ramadhan ni fursa adhimu kwa wananchi kwa ajili ya uchipuaji na ujengekaji kimaada na kimaanawi.

3701534

captcha