IQNA

Waislamu Austria wakasirishwa na mpango wa serikali wa "ramani ya Uislamu"

20:23 - May 30, 2021
Habari ID: 3473963
TEHRAN (IQNA)- Waislamu nchini Austria wamesema wana mpango wa kufungua kesi dhidi ya serikali ya Kansela Sebastian Kurz kwa kuanika "ramani ya Uislamu" iliyozusha utata mkubwa.

Jumuiya ya Vijana wa Kiislamu ya Austria (MJÖ) imeikosoa serikali ya nchi hiyo kwa kuchapisha kile ilichokiita "Ramani ya Uislamu", ambayo inaweka wazi maeneo ya misikiti na vyama vya Waislamu kote nchini humo.

Ripoti iliyotolewa na kundi hilo imesema imesema kuwa "uchapishaji na kuweka wazi majina, kazi na anwani za taasisi na jumuiya za Waislamu ni ukiukaji usio na kifani wa mipaka na sheria."

Jumuiya ya Dini ya Kiislamu nchini Austria (IGGO), ambayo inawakilisha Waislamu takribani 800,000,  pia imeonya dhidi ya kuwanyanyapaa Waislamu wanaoishi nchini humo na kusema hatua hiyo ni hatari kwa jamii na mfumo wa kidemokrasia nchini humo.

Taarifa hiyo imesema: "Kampeni hii inachochea ubaguzi na kuhatarisha usalama wa raia Waislamu."

Waziri wa Utangamano wa Austria, Susanne Raab Alkhamisi iliyopita alizindua wavuti inayoitwa Ramani ya Kitaifa ya Uislamu, ambayo ina majina na maeneo ya misikiti, jumuiya, na maafisa zaidi ya 620 Waislamu na mawasiliano yao nje ya nchi.

Itakumbukwa kuwa ripoti za mashambulio dhidi ya Waislamu nchini Austria zimeongezeka sana tangu shambulio la Vienna Novemba mwaka jana.

Hatua hiyo ya serikali ya Austria imepingwa vikali ndani na nje ya nchi hiyo. Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Uturuki imetoa taarifa ikisema: Sera za "chuki dhidi ya wageni, ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya Uislamu" zinahatarisha mshikamano wa kijamii na ushirikiano".

Taarifa hiyo imesema: "Ni muhimu kwa Austria kuacha kulenga wahamiaji na Waislamu kwa kuwatia "alama", na badala yake itekeleze sera za kuwajibika".

Askofu wa Kiinjili wa Kilutheri wa Ujerumani, Michael Chalupka pia ameeleza wasiwasi wake kuhusiana na hatua hiyo na amemtaka Raab aondoe tovuti hiyo.

Austria inakosolewa kwa kugeuka na kuwa kituo cha sera za chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya.

3474836/

Kishikizo: austria waislamu
captcha