IQNA

Sinwar: Mzingiro dhidi ya Ukanda wa Ghaza utavunjwa karibuni

16:48 - June 01, 2021
Habari ID: 3473968
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema wananchi wa Palestina wamekaribia sana kuuvunja mzingiro dhidi ya Ukanda wa Gaza uliowekwa na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kushirikiana na Misri tokea mwaka 2007.

Kiongozi wa HAMAS katika Ukanda wa Gaza, Yahya Sinwar alisema hayo jana Jumatatu katika mazungumzo yake na ujumbe wa Misri uliozitembelea ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.

Sinwar amenukuliwa na shirika la habari la Ma'an akisema kuwa, wananchi wa Palestina wamejitoa muhanga kwa ajili ya kadhia yao muhimu ya kujikomboa toka kwenye mzingiro na uvamizi wa utawala haramu wa Israel.

Amesisitiza kuwa, mazingira ya sasa ya kimataifa yameegemea zaidi kwa upande wa maslahi ya taifa la Palestina, na fursa hii inapaswa kutumiwa kwa njia bora zaidi.

Kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amebainisha kuwa, taifa la Palestina linastahiki kuishi na kujivunia haki zake za msingi. 

Kadhalika ametadharisha kuwa, wananchi wa Palestina wapo tayari kujibu aina yoyote ya uvamizi na chokochoko za utawala pandikizi wa Israel.

Tokea mwaka 2007, utawala haramu wa Israel, kwa kushirikiana na Misri, uliweka mzingiro wa anga, nchi kavu na baharini dhidi ya Ukanda wa Ghaza baada ya Wapalestina katika eneo hilo kuichagua kidemokrasia harakati ya Hamas kuongoza eneo hilo. Mzingiro huo umelifanya eneo hilo lenye watu karibu milioni moja na nusu kutajwa kuwa gereza kubwa zaidi la wazi duniani.

Mbali na mzingiro huo, utawala haramu wa Israel pia umeanzisha vita mara kadhaa dhidi ya Ghaza tokea mwaka 2008 ambapo maelfu ya Wapalestina wakiwemo wanawake na watoto wameuawa.

3474859

captcha