IQNA

Ibada ya Hija

Rais Samia azishauri Taasisi za Hija Tanzania

19:12 - May 17, 2022
Habari ID: 3475261
TEHRAN (IQNA)- TEHRAN (IQNA)- Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, ameziasa taasisi za Hija nchini humo, zinazosafirisha Mahujaji , kuacha tabia ya kuwalaghai Mahujaji.

Rais Samia ameyasema hayo mbele ya Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir, katika hotuba yake ya Baraza la Eid, lililofanyika Mei 3, 2022, katika Ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam.

Rais Samia amelazimika kutoa tahadhari hiyo kufuatia wito wa BAKWATA katika Baraza hilo la Eid kwa Waislamu waliotia nia ya Hija kufanya maandalizi ya kwemda Makka, kutekeleza nguzo ya Hija, kwa mwaka huu (2022).

Kwa miaka miwili Ibada ya Hjja, haikufanyika kwa Waislamu wa kutoka nje ya mipaka ya Saud Arabia, kutokana na mripuko wa ugonjwa wa COVID-19 au UVIKO 19.

Rais Samia, alisema, inatia moyo kusikia kwamba kwa mwaka huu 2022, kutokana na kupungua kwa maradhi ya UVIKO 19, kuna ruhusa ya watu kwenda Hija.

Lakini akasema, kwa kawaida Saudia, huwa inachukua Mahujaji takriban milioni mbili kwa dunia nzima, lakini mwaka huu wamefanya nusu yake kwa hiyo Tanzania, itakapopewa fursa zozote zile kwa uchache watakaopewa wazitumie kikamilifu nafasi hizo.

Rais Samia, alisema Hija ni Ibada hivyo wanaosimamia safari za Hija, waache tabia za kuchukua fedha za watu na kuwadanganya tena katika hali ngumu kama hii.

“Na niwaombe mnaosimamia hizi safari acheni hii tabia, Hija ni Ibada yenye uzito wa pekee katika maandalizi yake, sasa mnapochukua fedha za watu, kisha mkawadanganya tena katika hali ngumu kama hii, utakuta mtu amejikusuru amechanga vidola vyake kwa ajili ya safari.”

“Kisha baada ya hapo mnadanganya safari ipo siku ikifika hakuna safari, sasa kwa nafasi chache tutakazo pewa niwasihi manaoshughulikia safari za Hija kufanya uadilifu kwa kuhakikisha kila anaetoa senti yake anapata nafasi ya kwenda kufanya Ibada hii, niwasihi ndugu zangu tusicheze na suala hili,” amesema na kutahadhalisha Rais Samia.

Ama kuhusu suala la maadili, ambalo nalo liligusiwa katika salamu za Eid, ambapo BAKWATA ilieleza juu ya uwepo wa mmomonyoko wa maadili na ili kuikabili hali hiyo iliiomba serikali, kurasimisha somo la dini katika shule za serikali na kuajiri walimu wa dini ili watoto waanze kufundishwa misingi bora ya imani na uadilifu tangu wakiwa shule ya msingi hadi chuo kikuu.

Hii ni kwa sababu baraza hilo linaamini kuwa kwa ushirikiano wa pamoja baina ya wanadini, serikali na jamii kwa ujumla wanaweza kuliokoa taifa kutokana na mmomonyoko wa maadili ambao kila uchao unazidi kuota mizizi.

Akijibu ombi hilo Rais Samia, alikiri kuwepo kwa mmomonyoko wa maadili nchini, akasema nae ana amini kwamba wana dhima kubwa ndani ya nchi haswa kwa vijana wa kike na kiume.

Alisema, kwa jinsi wanavyosifia maendeleo na jinsi wanavyofungua nchi ndivyo tamaduni za kigeni zinavyoingia nchini kwa wingi.

“Niombe pamoja na ombi ya kwamba somo la dini lifundishwe mashuleni, watu wa serikali tupo hapa tunalichukua tatakwenda kuliangalia, lakini niombe pia kama wazazi kama walezi, tukae kwenye misingi ya kidini ya kimila na misingi ya tamaduni zetu katika kulea watoto wetu, kwani tumejisahau kidogo ukweli ni huo,” amesema Rais Samia.

Rais Samia, alisema kwa hali ilivyo sasa ni kwamba dunia ipo mbele na wazazi wapo nyuma na hata hao ‘panya road’ ni watoto waliozaliwa majumbani na wana dini zao lakini hawakukuzwa kwa misingi ya kidini.

Alisema na hilo ni kundi moja, lakini kuna makundi mengine ambayo ni fedheha hata kuyasema hapo kwa hiyo akawataka wazazi wa dini zote, Watanzania wote warudi kwenye misingi ya kidini mila na desturi zao katika kukuza watoto wao.

“Ni kweli kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili kwa watoto wetu kwa hiyo ni kazi yetu sisi kama wazazi kuwajibika. Vitabu vinatuambia kwamba wewe (mzazi) ni masu’ul, utakwenda kujibu kwa nini mtoto amekuwa ‘panya road,” amesema Rais Samia.

Awali Rais Samia, aliwashukuru Waislamu wote kwa Ibada na dua zilizokuwa zikifanyika na kuombwa ndani ya Mwezi wa Ramadhani.

Alisema, huo ndio mwenendo wanaotakiwa kwenda nao kwani akasema pamoja na jitihada wanazochukua za kulinda usalama, amani na utulivu ndani ya nchi kama si kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, utulivu huu hauwezi kuwepo kwa namna hii.

“Kwa hiyo Mwezi wa Ramadhani umepita tumejitahidi na Dua, naomba tuendelee kuomba kwani Dua hazina mwisho na hatujaambiwa kwenye kitabu chochote kwamba Dua ina mwisho ni vyema kuendelea kuomba Dua kwani Mungu amesema tukimuomba atatupa,” amesema Rais Samia.

Chanzo: Gazeti la Annuur

captcha