Ayatullah Ahmad Khatami amesema hayo katika khutba au hotuba za Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa Tehran na kuongeza kuwa,maadui wanafanya kila wawezalo ili kuzidogosha nukta mbili hizi katika mataifa ya Waislamu, ili wafanikishe njama zao za kuugawa umma wa Kiislamu.
Ayatullah Khatami ameongeza kuwa, ujumbe wenye thamani wa Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa Mahujaji unapaswa kuzingatiwa na kutathminiwa kwa wakati muafaka.
Moja ya nukta zilizoashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika ujumbe wake kwa Mahujaji ni kuwa, nchi za Magharibi zenye kiburi zimezidi kudhoofika siku baada ya siku katika eneo hili nyeti la Asia Magharibi, na hivi karibuni katika dunia nzima.
Kwingineko katika khutba zake, Ayatullah Khatami amesema maadui wanafanya juu chini kupunguza na kudhoofisha umoja wa umma wa Kiislamu kwa kutumia mbinu mbalimbali. Ameongeza kuwa, baadhi ya mbinu zinazotumiwa na maadui kuyumbisha umoja wa Waislamu ni kujaribu kuwapotosha waachane na masuala ya kimaanawi na kumkumbuka Allah.