Imam Ridha AS ni kiongozi ambaye kwa
zaidi ya miaka 1000 iliyopita aliingia katika ardhi ya Iran na kufuatia ujio
wake huo, wapenzi wa Mtume na Ahlu Bait wake AS wakajaa furaha na msisimko.
Katika siku kama hii nyoyo zote zimeelekea katika haram ya Imam Ridha AS. Licha
ya kupita karne nyingi lakini bado wapenzi na wafuasi wa mtukufu huyo kutoka
pembe zote za dunia humiminika kwa wingi katika mji mtakatafu wa Mash'had
ulioko kaskazini mashariki mwa Iran ili wapate kupitisha masaa na siku chache
katika mji huo mtakatifu kwa madhumuni ya kukata kiu yao ya kimaanawi kwa
kuzuru kaburi takatifu la mjukuu huyo wa Mtume SAW.
Wimbi hili kubwa la wapenzi wanaomzuru Imam Ridha AS linakumbusha zama ambazo
Imam alitoka katika mji mtakatifu wa Madina kuelekea katika ardhi ya Marw
nchini Iran. Msafara mkubwa ulikuwa unapita katika mji wa Neishabur hapa Iran,
ambapo kwa siku kadhaa wakazi wake walikuwa wamejitayarisha kwa lengo la
kumkaribisha Imam. Wakati msafara ulipoingia mjini hapo watu walianza
kunong'onezana na hapo machozi ya furaha na upendo yakaanza kuwabubujika. Kila
mtu alianza kudhihirisha hisia zake kwa njia tofauti. Makaribisho ya wakazi wa
mji huo yalikuwa makubwa kiasi kwamba msafara ulilazimika kusimama. Wote
walikuwa na hamu kubwa ya kuona na kumsikia Imam akizungumza, ambapo alitumia
fursa hiyo kuwahutubia.
Katika mazingira hayo ya kimya kikubwa, Imam AS aliwanukulia hadithi ambayo
Mwenyezi Mungu alimuhutubu Mtume wake SAW kwa kusema: 'Kalima ya la ilaha
Illallah ni ngome yangu, na kila mtu anayeingia katika ngome hii, huwa
amesalimika kutokana na adhabu yangu.' Baada ya kusoma hadithi hiyo Imam Ridha
AS alisema kuwa yeye pia ni sharti la kuingia kwenye ngome hiyo. Alisema:
'Lakini kwa kuzingatia masharti yake na mimi ni moja ya masharti hayo.' Kwa
maneno hayo, Imam Ridha AS alibainisha wazi nafasi muhimu ya Ahlul Beit AS
ambapo yeye ni mmoja wao, katika kuongoza umma wa Kiislamu.
Sisi pia tunazielekeza nyoyo zetu kwenye ugeni wa haram angavu ya Imam Ridha na
kumtumia salama kwa kusema: 'Salamu ziwe juu yako ewe Ali bin Musa ar-Ridha AS
! Salamu ziwe juu yako ewe mjukuu mtakatifu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu! Salamu
za dhati za waumini wote wa dunia ziwe juu ya uwepo wako ewe chemchemi ya
maarifa na hekima!
Imam Ridha (as) alizaliwa mwaka 148 Hijiria sawa na 765 Miladia katika mji
matakatifu wa Madina. Baada ya kupata mafunzo na kulelewa na baba yake mtukufu
Imam Musa Kadhim AS Imam alikuwa tayari kubeba jukumu zito la kuuongoza umma wa
Kiislamu. Alikuwa chemchemi ya elimu na fadhila. Aliridhia uamuzi wa Mwenyezi
Mungu katika kila kitendo na neno alilosema. Ni kutokana na sifa hiyo ndipo
akaitwa kwa lakabu ya Ridha, yaani mtu anayeridhia kila jambo linalotoka kwa
Mwenyezi Mungu. Imam Ridha aliwaongoza Waislamu kwa muda wa miaka 20 ambapo
sehemu kubwa ya uongozi huo ulitimia mjini Madina na kumalizia miaka mitatu ya
uimamu wake akiwa mjini Marw katika ardhi ya Khorasan. Imam alilazimishwa na
Ma'mun, mtawala wa ukoo wa Bani Abbas kuuhama mji wa Madina na kuelekea Marw
yaliyokuwa makao makuu ya utawala wao. Katika zama hizo, Marw ulikuwa kituo cha
elimu cha Khorasan. Imam pia alitumia fursa hiyo na kuanzisha harakati kubwa ya
kielimu. Kutokana na maslahi ya kisiasa, Ma'mun alijaribu kujikurubisha kwa
Imam AS lakini wakati huohuo akifanya njama za kudhoofisha shakhsia yake ya
kielimu kwa kuandaa mihadhara na mijadala ya kielimu ya wanazuoni. Imam (as)
alikuwa akiwashinda wasomi mashuhuri katika mijadala hiyo na kuwaathiri pakubwa
kutokana na elimu kubwa na hoja za nguvu na madhubuti alizokuwa akizitumia
katika mijadala hiyo.
Uislamu ni dini ambayo inakaribisha maswali tofauti na hakuna hata sehemu moja
ambapo Maimamu (as) wamewahi kuulizwa swali na kukataa au kukwepa kulijibu.
Imam Ridha AS pia ambaye alibeba jukumu zito la kuuongoza umma wa Kiislamu
daima alikuwa akikaribisha maswali kutoka kwa wengine na kuwa tayari kushiriki
kwenye mijadala mbalimbali ya kielimu. Mijadala ya kielimu ya Imam Ridha (as)
ilikuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha na kueneza utamaduni wa Kiislamu.
Katika mijadala hiyo Imam (as) alikuwa na lengo la kuwaongoza watu na kamwe
hakufikiria juu ya kushindana wala kujiona kuwa mbora zaidi. Alikuwa akitumia
mbinu za hoja kuthibitisha ukweli wa itikadi za Kiislamu kwa sababu migongano
ya kifikra haiwezi kuondolewa bila kutumiwa hoja za kifikra. Imam AS alikuwa
akisema: 'Iwapo watu watajua uzuri na ladha ya maneno yetu Ahlul Bait bila
shaka watatufuata.' Ni mazungumzo na mijadala hiyohiyo ya kielimu ndiyo iliyokuwa
ikiwabadilisha maadui wa Maimamu kuwa marafiki.
Imam Ridha AS ambaye alikuwa akifahamu vyema mbinu za majadiliano alikuwa
akiheshimu na kufuata sheria zote za majadiliano. Uzingatiaji wa viwango vya
utamaduni katika zama hizo na kuchaguliwa ibara na maneno yanayofaa kwa
kuzingatia uwezo wa kifikra na kielimu wa upande wa pili ni mambo yaliyokuwa
yakipewa umuhimu mkubwa na Imam AS katika mijadala yake. Katika mijadala yake
na Wakristo alikuwa akizingatia imani na masuala ya pamoja na kutumia hoja
zinazokubaliwa na Wakristo hao katika kuthibitisha ukweli wa imani ya Kiislamu.
Licha ya kuwa na kiwango kikubwa cha elimu lakini Imam hakuthubutu kuudunisha
wala kudhalilisha upande wa pili katika mijadala yake ya kielimu. Imam alikuwa
akiwaheshimu watu wote bila kujali imani, rangi na dini zao. Tunaona katika
mjadala wake na mtu mmoja ambaye hakumwamini Mwenyezi Mungu kwa jina la Imran
as-Sabi kwamba tabia nzuri na ya kuvutia ya Imam pamoja na hoja zake madhubuti
za kuthibitisha mambo zilimpelekea mtu huyo kusilimu na kumwamini Imam AS.
Katika kipindi chote cha mjadala wao Imam alikuwa akimwita Sabi kwa jina lake
la mwanzo jambo ambalo bila shaka lilikuwa na athari kubwa katika kujenga
urafiki na kumuondolea hali ya hofu na woga mbele ya Imam AS. Katika kujibu maswali
ya Imrani as-Sabi Imam alikuwa akimuuliza: 'Je, umeelewa ewe Imran?' Tabia hiyo
ya kuvutia ya Imam ilimfanya pia Imran amjibu Imam kwa heshima kwa kusema: 'Nam
bwana wangu.'
Lengo la mjadala linapasa kuwa ni kufikiwa ukweli na lengo hilo huthibiti pale mjadala
unapofanyika mbali na taasubi na uadui usio na msingi. Kutokana na kuwa na
maadili ya hali ya juu, Imam hakuwahi kuutuhumu upande wa pili kwa kusema uongo
na wala hakuwahi kutaja jambo ambalo lingepelekea upande wa pili kuhisi kuwa
unadharauliwa na kudhalilishwa. Daima alikuwa akikosoa kosoro za kiitikadi na
kifikra na wala sio shakhsia ya watu aliokuwa akijadiliana nao. Mihadhara na
mijadala ya Imam Ridha AS ilikuwa na baraka nyingi kwa ulimwengu wa Kiislamu,
kukiwemo kuthibitishwa kwa moyo wa uhuru kwenye Uislamu. Katika mijadala hiyo
Imam AS alithibitisha kwamba Uislamu haukuenezwa duniani kwa mabavu na ncha ya
upanga kama wanavyodai maadui na waongo, na alitoa mfano wa wazi jinsi kiongozi
mkubwa wa Kiislamu anavyowapa wapinzani wake fursa ya kukosoa na kutoa mitazamo
yao kuhusu masuala tofauti hata kama itakuwa ni ya kupinga Uislamu na Tauhidi,
bila ya kuhofu wala kuogopa lolote. Baraka nyingine za mijadala hiyo ni kuwa
Imam Ridha AS aliitumia vyema katika kueneza maarifa ya Kiislamu na kufunga njia
za wapinzani na maadui waliotaka kuidhuru dini hii tukufu. Alitumia mihadhara
hiyo kufichua njama zilizokuwa zikifanywa na maadui kwa ajili ya kupotosha
Uislamu sahihi kwa kunukuu elimu za wageni na kuzisambaza kwenye Uislamu.
Ni matumaini yetu kwamba sote tutafuata mbinu na njia hii ya Mtume AS na Ahlul
Bait wake AS katika kumulika njia ya Waislamu katika zama zote. Kwa mara
nyingine tena tunatoa mkono wa pongezi na fanaka kwa Waislamu wote duniani na
hasa wafuasi wa Ahlul Beit AS kwa mnasaba huu adhimu wa kuadhimishwa uzawa wa
Imam Ridha AS.