Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kuwafuata sawasawa Maimamu maasumu ni kuwafuata kivitendo watukufu hao na kudumisha mapambano dhidi ya ukafiri na unafiki. Ameongeza kuwa: Mapambano dhidi ya ukafiri na unafiki wa kimataifa ni rahisi na jambo linalowezekana katika Jamhuri ya Kiislamu lakini tangazo lolote la kujibari na kujitenga na Marekani chini ya kivuli kiovu cha baadhi ya tawala za eneo la Mashariki ya Kati hufuatiwa na hasira na jibu kali la tawala hizo.
Ayatullah Khamenei amesema, mapambano dhidi ya madhalimu hayahusu tu mapambano ya kutumia silaha na upanga na kwamba hii leo suala la kulingania dini duniani linachukua nafasi ya kwanza na inawezekana kupambana na madhalimu kwa kutumia maneno na mashairi. Amesisitiza kuwa, katika miaka ya hivi karibuni kumeshuhudiwa mifano mizuri sana na ya kutia matumaini katika uwanja huo.
Suala la mtindo wa maisha na wajibu wa malenga na washairi wa kidini mkabala wake, ni miongoni mwa masuala yaliyoashiriwa na Kiongozi Muadhamu katika mkutano huo. Amesema kuwa: Hii leo barani Ulaya na Marekani kumeanzishwa vituo na taasisi zenye malengo maalumu kwa ajili ya kubadili mtindo wa maisha katika nchi zisizo za Kimagharibi hususan Iran ya Kiislamu.
Ayatullah Khamenei amesema lengo la hujuma inayofanywa dhidi ya
mtindo wa maisha wa Kiislamu ni kuanzisha irada, azma na harakati
inayoowana na matakwa ya taasisi za Kimagharibi. Ameongeza kuwa, mkabala
wa hujuma hiyo, haitoshi kujihami na kujiwekea uzio, bali tunaweza
kutekeleza majikumu yetu kwa kubainisha na kuweka wazi mtindo wa maisha
wa Kiislamu na kueleza mafundisho na misingi ya kimaadili, kisiasa na
kiutamaduni katika kalibu na sura ya mashairi.