IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

Rais wa Chechnya atangaza zawadi kwa atakayemkamata askari wa Ukraine aliyeivunjia heshima Qur'ani

22:01 - March 19, 2023
Habari ID: 3476730
TEHRAN (IQNA)- Rais Ramzan Akhmadovich Kadyrov, Jamhuri ya Chechnya yenye mamlaka ya ndani katika Shirikisho la Russia ametenga zawadi ya Ruble milioni 10 za Kirusi ambazo ni sawa na dola 168,000 za Kimarekani kwa atakayefanikisha kukamatwa akiwa hai, askari wa jeshi la Ukraine aliyeivunjia heshima Qur'ani tukufu kwa kuichoma moto nakala ya kitabu hicho kitakatifu.
Tovuti ya kituo cha habari cha Rusiya Al-Yaum imeripoti kuwa, Kadyrov ametenga pia ruble milioni tano kwa mtu atakayeweza kuukabidhi mwili wa mwanajeshi huyo aliyeivunjia heshima Qur'ani tukufu.
Rais wa Chechnya ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa telegram: "sitatosheka na kulaani tu kitendo cha askari wa Ukraine, ambao hivi karibuni walizichoma moto kurasa za Qur'ani."
Kadyrov ameongezea kwa kusema: "mukiona kwenye ukurasa wangu wa telegram taswira za kitendo hiki kiovu, mujue kwamba, ninatangaza zawadi yenye thamani ya ruble milioni tano kwa ajili ya kuwaangamiza watu hawa; na mara mbili yake kwa kuwakamata wakiwa hai. Na tuzo hii ya fedha itabaki kama ilivyo bila kujali kama takwa hili litafanikishwa leo, kesho au hata mwaka ujao".

Rais wa Chechnya amemhutubu mwanajeshi huyo wa Ukraine kuwa ni mtu mwoga na kumwambia: "ewe uliyefunika uso wako kwa woga na hofu, fahamu kwamba popote utapokuwa umejificha utaadhibiwa tu; na nafsi yako iliyojaa woga katu haitapata amani na utulivu".

Wanajeshi kadhaa wa jeshi la Ukraine wenye misiamamo ya kufurutu mpaka wamefanya kitendo kiovu na cha kifidhuli kwa kusambaza kwenye mitandao ya kijamii video inayowaonyesha wakirarua na kuzichoma moto kurasa za nakala ya Qu'rani tukufu.
Wakati wakifanya kitendo hicho kiovu, askari hao wa jeshi la Ukraine wanaonekana pia wakitoa maneno ya matusi kuhusiana na Qur'ani, huku mmoja wao akisaga na kumimina shahamu ya nguruwe kwenye nakala hiyo ya Qur'ani Tukufu.
Wakati huo huo, Wizara ya Wakfu ya Syria imelaani vikali kitendo cha kuchomwa moto nakala ya Qur'ani Tukufu nchini Ukraine, na kutangaza kwamba hatua hiyo imetekelezwa kwa lengo la "kugeuza vita vya kisiasa kuwa vita vya kidini".

Sheikh Khizr Shahrour, mwakilishi wa Waziri wa Wakfu wa Syria amesema kuwa, Waislamu wote duniani wanalaani kitendo cha kuchomwa moto Qur'ani Tukufu kilichofanywa na jeshi la Ukraine, na kukivunjia heshima Kitabu cha Mwenyezi Mungu ni tabia na mwenendo mchafu unayosababisha chuki.

Sheikh Khizr Shahrour ameongeza kuwa, kimya cha serikali ya Ukraine mbele ya kitendo hicho kiovu cha wanajeshi wake ni ishara ya kuridhia kitendo hicho na kubadilisha mkondo wa vita hivyo chini ya uongozi wa Marekani kuwa vita vya kidini vinavyopingwa na wanasiasa wenye busara.

Mwakilishi huyo wa Waziri wa Wakfu wa Syria amesisitiza kuwa, Wamagharibi ndio walioanzisha misimamo mikali na ya kuchupa mipaka na wala sio Waislamu, na kwamba ni Wamagharibi pia ndio walioasisi ugaidi na kuusambaza katika maeneo mengine ya dunia. 

4128721

captcha