IQNA

Afisa wa Nigeria: Wanawake wa Kiislamu wana haki ya kuvaa Hijabu

17:49 - February 07, 2022
Habari ID: 3474903
TEHRAN (IQNA)- Katiba ya Nigeria inaruhusu wanawake wa Kiislamu kuvaa Hijabu kulingana na mafundisho ya imani yao, waziri wa elimu wa nchi hiyo ya Kiafrika alisema.

Adamu Adamu alibainisha kuwa wananchi wote wanaruhusiwa kufuata dini zao ilimradi tu hakuna madhara au usumbufu utakaotokea kwa watu wengine.

Aliyasema hayo katika Msikiti wa Kitaifa, Abuja, siku ya Jumapili katika hotuba ya hadhara iliyoandaliwa na Muungano wa Wanawake wa Kiislamu wa Nigeria kama sehemu ya shughuli za kuadhimisha Siku ya Hijabu Duniani mwaka huu.

Adamu, akiwakilishwa na Hajiya Sidikat Shomope wa Idara ya Uhamasishaji Jamii, Tume ya Elimu ya Msingi kwa Wote (UBEC), alisema inasikitisha kwamba mabishano ya uvaaji wa Hijabu nchini Nigeria yameshuka hadi katika ngazi ya shule na kuzua malumbani o yasiyo na sababu.

Kulikuwa na vurugu siku ya Alhamisi katika Shule ya Upili ya Baptist, Ijagbo katika Serikali ya Mtaa ya Oyun Jimbo la Kwara, na kusababisha kuuawa kwa Habeeb Idris, mwanafunzi Mwislamu wa shule hiyo, wakati mkutano wa wanafunzi Waislamu uliripotiwa kuvurugwa na vibaka na maafisa wa usalama. .

Waziri huyo alisema uvaaji wa hijabu kwa wanawake wa Kiislamu ni wajibu kwa mujibu wa mafundisho ya Quran Tukufu.

Kulingana naye, kuna mengi ambayo nchi inaweza kupata kwa mazungumzo juu ya maswala ya tofauti za kidini badala ya kufanya vurugu.

"Watoto wetu watasalia kuwa raia wa Nigeria bila kujali imani zao. Wataishi na kuingiliana katika ulimwengu nje ya shule ambapo hakuna mpaka kati ya dini.

"Tunapaswa kuelewa kwamba katiba ya Shirikisho la Jamhuri ya Nigeria inahakikisha uhuru wa dini kwa raia wote. Hilo linamaanisha kwamba raia wote wanaruhusiwa kufuata dini zao kulingana na mafundisho ya imani yao maadamu tu hakuna madhara au usumbufu unaosababishwa kwa watu wengine.”

Alitoa wito kwa viongozi wote wa kimila, dini na jamii kutumia ofisi zao kupunguza hali ya wasiwasi na taharuki ili wananchi wa Nigeria waishi kwa amani, utangamano na kuvumiliana.

Adamu pia alitoa wito kwa wazazi na walimu wa shule “kuhakikisha kwamba kwa maneno na matendo, wanatoa kielelezo bora kwa watoto wetu cha kuiga.”

3477719

Kishikizo: nigeria abuja hijabu
captcha