IQNA

Shujaa Muislamu

Kijana wa Kiislamu aenziwa kwa ujasiri wa uokoaji wa watu 100+ katika hujuma ya kigaidi Moscow

11:19 - March 28, 2024
Habari ID: 3478595
IQNA - Kijana wa Kiislamu ambaye aliokoa zaidi ya watu 100 wakati wa shambulio la kigaidi dhidi ya ukumbi wa tamasha mjini Moscow, ameendelea kupongezwa na kuenziwa.

Maria Lvova-Belova, Mkuu wa Haki za Watoto Russia, alimtunuku diploma ya heshima Islam Khalilov mwenye umri wa miaka 15 siku ya Jumanne kwa "kujitolea, ujasiri na ushujaa wa kibinafsi."

Lvova-Belova alitembelea shule ya Khalilov kuwasilisha tuzo hiyo katika sherehe kubwa. Khalilov alikuwa akifanya kazi kwa muda kama mhudumu wa chumba cha nguo katika ukumbi wa tamasha wa Crocus wakati ufyatuaji risasi ulipoanza. Alipoona watu wakiwa na hofu na kuchanganyikiwa, alichukua jukumu, akatangaza kuwa yeye ni mfanyakazi na kuwaongoza hadi njia za kutoka.

Licha ya kuwa katika hatari kubwa, Khalilov alikuwa amedhamiria kuhakikisha hakuna mtu anayeachwa nyuma. Katika sherehe ya tuzo, alisifu malezi yake kwa matendo yake, akisema, "Baba amekuwa akisema kila wakati kwamba ikiwa unaweza kusaidia kwa njia yoyote, saidia watu kila wakati." Pia alieleza kuwa amepokea jumbe nyingi kwenye mitandao ya kijamii kutoka kwa watu wakimshukuru kwa kuokoa maisha ya jamaa zao.

Lvova-Belova alisifu vitendo vya Khalilov, akisema, "Hii inashangaza kwani yeye kama mtoto alihitaji kuokolewa menyewe lakini akachukua jukumu la kuokoa watu."

Shambulio hilo katika Jumba la Jiji la Crocus huko Krasnogorsk, Mkoa wa Moscow, mnamo Machi 22 lilisababisha vifo vya watu 139 na zaidi ya 180 kujeruhiwa. Kamati ya Uchunguzi iliwakamata watu 11, wakiwemo wahusika wanne, katika eneo la mpaka wa Bryansk walipokuwa wakielekea nchi jirani ya Ukraine. Jumapili, Mahakama ya Wilaya ya Basmanny ya Moscow iliwashtaki wanne hao kwa ugaidi na kuidhinisha kuzuiliwa kwao kabla ya kusikilizwa kwa kesi hadi Mei 22.

Kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) limedai kuhusika na hujuma hiyo ya kigaidi ambayo inaendelea kulaaniwa duniani kote. Hatahivyo wakuu wa Russia wanasisitza kuwa madola ya Magharibi yalihusika na hujuma hiyo.

Video iliyosambaa mitandaoni inaonyesha watu wanne waliojizatiti kwa bunduki ya otomatiki wakiwamiminia risasi watu waliokuwa wamekusanyika kwenye ukumbi wa tamasha kwenye viunga vya mji wa Moscow, dakika dakika chache baada ya kujiri mripuko na moto mkubwa kusambaa ukumbini hapo.

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump katika kampeni zake za kuwania urais aliwahi kusema kuwa kundi la kigaidi la Daesh liliasisiwa na rais wa zamani wa nchi hiyo Barack Obama. Kundi hilo limehusika na vitendo vya kigaidi na kuua maelfu ya watu wasio na hatia duniani kote. Serikali ya Russia imekuwa mstari wa mbele kupambana na magaidi wa Daesh nchini Syria na imeweza kufanikiwa kuwaangamiza magaidi hao katika nchi hiyo ya Kiarabu.

3487732

Kishikizo: Moscow isis daesh
captcha