IQNA

Kamishna wa Haki za Binadamu UN ataka dunia ishinikize Myanmarisitishe ukatili

15:29 - January 30, 2022
Habari ID: 3474869
TEHRAN (IQNA)- Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet ameitaka jamii ya kimataifa izidishe mashinikizo kwa jeshi la Myanmar ili likomeshe kampeni yake ya ukatili na ukandamizaji dhidi ya watu wa Myanmar na kusisitiza kurejeshwa mara moja utawala wa kiraia nchini humo.

Bi Bachelet amesema, "ninaziomba serikali katika kanda hii na kwingineko kusikiliza ombi hili. Ni wakati wa juhudi za haraka na mpya za kurejesha haki za binadamu na demokrasia nchini Myanmar na kuhakikisha kwamba wahusika wa ukiukwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa utaratibu wanachukuliwa hatua.” 

Kamishna mkuu huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, wiki hii amezungumza ana kwa ana na watetezi wa haki za binadamu "wenye dhamira na jasiri" ambao wanaisihi jamii ya kimataifa isiwaache mkono, bali ichukue hatua madhubuti kuhakikisha haki zao zinalindwa na jeshi la Myanmar linawajibishwa. 

Bachelet amebainisha kuwa, amesikia habari za kutisha za ukiukaji wa haki, kama vile waandishi wa habari kuteswa; wafanyakazi wa viwandani kutishwa, kunyamazishwa na kunyonywa; na kuzidishwa mateso dhidi ya makabila madogo na ya kidini, wakiwemo Waislamu Warohingya. 

Pamoja na hayo, "watetezi wa haki za binadamu wenye ujasiri na wanaharakati wa vyama vya wafanyakazi wanaendelea kuandamana, kutetea, kuandika na kukusanya ushahidi unaoongezeka wa ukiukaji wa haki za binadamu," amesema kamishna huyo wa haki za binadamu wa UN.

Tangu jeshi lilipochukua mamlaka mwezi Februari mwaka jana, vikosi vya usalama nchini Myanmar vimejaribu kuzima upinzani, na kusababisha vifo vya watu 1,500: idadi ambayo haijumuishi maelfu ya waliouawa katika vita na ghasia ambazo zimeongezeka nchini kote. 

Takriban watu 12,000 wamewekwa kizuizini kiholela kwa kutoa maoni yao dhidi ya jeshi, ama katika maandamano ya amani au mtandaoni. Takriban watu 8,792 wamesalia kizuizini, na takriban 290 wamekufa wakiwa kizuizini, pengine kutokana na matumizi ya mateso.

4032157

Kishikizo: myanmar waislamu
captcha