IQNA

Wazayuni wazidisha jinai, karibu watu 1,700 wameshauawa shahidi Ghaza

19:40 - August 02, 2014
Habari ID: 1435159
Duru za habari katika Ukanda wa Ghaza zinaarifu kuwa, karibu Wapalestina 1,700 wameshauawa shahidi katika jinai za siku 27 mtawalia za utawala huo katili wa Kizayuni kwenye ukanda huo.

Habari zinasema kuwa, idadi ya wahanga imeongezeka baada ya jeshi la utawala huo pandikizi kuvunja makubaliano ya usitishaji vita kwa masaa 72, yaliyokuwa yametangazwa na Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Marekani. Inaelezwa kuwa, baada muqawama wa Palestina kuanza kutekeleza makubaliano hayo ya usitishaji vita, raia wa Ghaza walianza kuelekea makwao sambamba na kuanza kuwaokoa watu waliofukiwa katika vifusi vya nyumba zilizoshambuliwa na jeshi hilo katili, hata hivyo Israel ilitumia fursa hiyo kuwashambulia raia wasio na hatia katika maeneo tofauti ya Ukanda wa Ghaza hapo jana na kuua shahidi zaidi ya watu 120 katika kipindi cha siku moja pekee. Eneo la Rafah ndilo lililoshuhudia jinai kubwa zaidi za Wazayuni hapo jana. Mashambulizi ya utawala huo yameendelea pia usiku mzima uliopita. Weledi wa mambo wazitaja jinai za utawala wa Kizayuni huko Ghaza kuwa ni sawa na jinai zilizotendwa na Hitler wa Ujerumani enzi za uhai wake.
Muqawama wamteka askari wa Kizayuni, Israel yakiri
Wanamapambano wa Kipalestina, wamefanikiwa kumteka nyara askari mwengine wa ngazi za juu wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza. Habari zinasema kuwa, jana askari wa Kizayuni waliingia katika eneo la Karm Abu Salem huko Ghaza ambapo bila kufahamu walijikuta wameingia kwenye mtego wakiwa wamezingirwa na wanamapambano wa Kipalestina na kuuliwa kwa mpigo huku askari huyo mwenye nafasi ya juu jeshini akitiwa mikonini mwa Wapalestina hao na kwenda naye kusikojulikana. Tayari jeshi la utawala haramu wa Kizayuni limekiri kupotea moja ya askari wake katika eneo la Karm Abu Salem ambalo lipo karibu na Rafah. Kufuatia hali hiyo, Brigedi ya Izzuddin Qassam tawi la kijeshi la Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa Palestina Hamas imewaonya askari wa Kizayuni kutotenda kosa la kuingia katika eneo la Ghaza na kwamba ikiwa watathubutu kufanya hivyo basi watakiona cha mtema kuni.
Juhudi za Iran za kusitisha jinai za Israel Ghaza
Kikao cha dharura cha kamati ya pamoja ya uratibu ya nchi wanachama wa harakati ya nchi zisizofungamana na siasa za upande wowote (NAM), kundi la 77 pamoja na China kimefanyika chini ya uwenyekiti wa Gholam-Hossein Dehqani, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa. Kikao hicho cha dharura kimefanyika kufuatia kuendelea kwa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Ukanda wa Ghaza sambamba na kuibuka maafa ya kibinadamu katika eneo hilo. Iran imeitisha kikao hicho katika juhudi za kukomesha jinai za utawala wa Kizayuni huko Ghaza.
Nchi wanachama wa kamati ya pamoja ya uratibu ya NAM zimetoa azimio na kulaani mashambulizi ya kijeshi ya Israel katika Ukanda wa Ghaza. Wajumbe wa kamati hiyo pia wameashiria hatua za uharibifu za wanajeshi wa utawala wa Kizayuni za kubomoa nyumba za raia wa Palestina na miundo mbinu muhimu ya mji vikiwemo vyanzo vya maji safi na taka zilizoshadidisha hali mbaya ya mambo katika Ukanda wa Ghaza na kuwazidishia masaibu raia wa Kipalestina milioni 1.8 wa eneo hilo, na kubainisha wasiwasi wao kutokana na hali hiyo na kutaka kutolewa haraka iwezekanavyo misaada ya kibinadamu kwa ajili ya raia hao wa Kipalestina.

1434932

Kishikizo: ghaza palestina kizayuni
captcha