IQNA

Utakfiri na misiamo mikali kwa mtazamo wa Wanazuoni wa Kiislamu

13:29 - November 24, 2014
Habari ID: 2611223
Kongamano la Kimataifa la ‘Hatari ya Misimamo Mikali Na Utakfiri Kwa Mtazamo wa Maulamaa wa Kiislamu’ lilianza jana hapa nchini Iran katika mji Mtakatifu wa Qum kusini mwa Tehran kwa kuhuduriwa na mamia ya maulamaa na wanafikra wa Kiislamu kutoka madhehebu ya Shia na Sunni.

Katika kongamano hilo la siku mbili, wanazuoni wa Kiislamu watabainisha mtazamo wao kuhusu utambulisho na hatari ya makundi ya Kitakfiri. Katika mijadala yao, wanazuoni hao wa Kiislamu wamelenga kuzingatia nukta nne ambazo ni pamojha na kuchunguza mizizi ya matakfiri na itikadi zao, utakfiri na mielekeo ya kisiasa na njia muafaka za Waislamu kujikwamua kutokana na utakfiri.

Akizungumza katika ufunguzi wa kongamano hilo, Ayatullah Nasser Makarim Shirazi mwanazuoni wa ngazi za juu wa Kiislamu amesema Maulamaa wa ulimwengu wa Kiislamu wanalenga kukausha mizizi ya fikra za utakfiri. Ayatullah Makarim Shirazi ameongeza kuwa makundi ya kitakfiri yametoa pigo kubwa kwa Uislamu na Waislamu na pia kwa wanaadamu. Mwanazuoni huyo mwandamizi amesema ni wadhifa wa nchi za Kiislamu kukabiliana na malengo ya pote potofu la matakfiri. Ayatullah Makarim Shirazi ambaye pia ni Marjaa Taqlid wa Mashia ameongeza kuwa Uislamu ni dini ya mapenzi na ukarimu lakini makundi ya kitakfiri yanaonyesha taswira potofu ya Uislamu na kuiarifisha dini hii tukufu kama dini ya umwagaji damu. Ameendelea kusema kuwa Uislamu hauna uhusiano wowote na makundi ya Kitakfiri na hivyo maulamaa wa Kiislamu wanapaswa kung'oa mzizizi wa fitina ya matakfiri. Ayatullah Makarim Shirazi ameongeza kuwa, Mwenyezi Mungu SWT katika Qur’ani Tukufu na Mtume Mtukufu wa Uislamu Mohammad SAW wamesisitiza kuhusu umuhimu wa kulindwa maisha na heshima ya Waislamu lakini la kusikitisha ni kuwa makundi ya matakfiri pasina kuzingatia kuwa Uislamu ni dini ya rahma wameharibu sura ya Uislamu duniani kwa vitendo vyao viovu.

Akihutubu katika kongamano hilo Ayatullah Ahmad Jannati Mkuu wa Baraza la Kulinda Katiba ya Iran amesema leo uwepo wa Uislamu ikiwa ni pamoja na madhehebu yote ya Waislamu iwe ni Masunni na Mashia uko hatarini kutokana na mrengo potofu wa matakfiri na wenye misimamo mikali. Mwanazuoni huyo ambaye pia ni khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa Tehran ameongeza kuwa, ‘ulimwengu wa Kiislamu umehisi hatari kutokana na kuenea Mawahabbi matakfiri kwani wanaleta mifarakano na kuwagonganisha Waislamu. Ayatullah Jannati amesisitiza kuwa Waislamu wote wanapaswa kukabiliana na magaidi kwani magaidi wa kitakfiri hawatumii mantiki na hivyo wanapaswa kuchukuliwa hatua za kivitendo.

Kongamano la Kimataifa la ‘Hatari ya Misimamo Mikali Na Utakfiri Kwa Mtazamo wa Maulamaa wa Kiislamu’ pia limehutubiwa na Dkt. Ibrahim Ja’afari Waziri wa Mambo ya Nje ya Iraq ambaye amesema, ‘Matakfiri ni tishio kwa ulimwengu kutokana na kuwa wanaeneza Uislamu bandia.’ Ameendelea kusema kuwa Magaidi hawana dini wala dhehebu na kwamba hakuna shaka kuwa matakfiri hawamuonei huruma mwanaadamu yeyote isipokuwa wale wanaofuata itikadi zao potofu. Ja’afari amesisitiza kuhusu kuyafahamu kwa usahihi makundi ya kitakfiri na kuongeza kuwa, ‘utamaduni wa ugaidi na utakfiri ni utamaduni unaohalalisha kuuawa Waislamu na kuporwa mali zao kutokana na vijisabau vidogo vidogo na ni kwa msingi huo ndio makundi kama vile Daesh (ISIL) yakaibuka. Naye Sheikh Abdullah Katamto, Naibu Mkuu wa Umoja wa Maulamaa wa "Biladush Sham" amesema kuwa fikra za vijana wanaojiunga na makundi ya Mawahabi  wa kitakfiri na kigaidi zinatumikia malengo ya mabeberu na kwamba Waislamu wanapaswa kushikamana chini ya mwavuli wa mafundisho matukufu ya Qur'ani na ya Bwana Mtume Muhammad SAW.

Kongamano la Kimataifa la ‘Hatari ya Misimamo Mikali Na Utakfiri Kwa Mtazamo wa Maulamaa wa Kiislamu’ linahudhuriwa na maulamaa zaidi ya 300 wa Kishia na Kisuni kutoka takribani nchi 83 za kigeni huku Iran ikiwakilishwa na Maulamaa 500 wa Kishia na Kisuni.../mh

2610960

captcha