IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Iran imestawi katika teknolojia za Nano na Bioteknolojia

10:02 - February 01, 2015
Habari ID: 2792669
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei, amesema mafanikio makubwa yaliyopatikana katika teknolojia ya Nano na Bioteknolojia ni mfano na kipimo cha maendeleo katika sekta mbalimbali nchini

Ameongeza kwamba mafanikio hayo yanaonyesha kuwa ikiwa majimui ya wataalamu wa fani maalumu, wenye mapenzi na uchungu wa nchi watashughulikia jambo kwa umakinifu, maendeleo ya kasi na yenye kuonekana yatapatikana. Ayatullah Khamenei ameyasema hayo Jumamosi asubuhi mjini Tehran mbele ya hadhara ya wahadhiri, watafiti na waendeshaji wa sekta ya teknolojia ya Nano na Bioteknolojia ambapo alisisitiza juu ya kuendelezwa ustawi wa elimu nchini na kubainisha sababu zilizowezesha kupatikana maendeleo ya kisayansi hususan katika sekta ya Nano. Amesema, “mipango makini”, “uthabiti katika uongozi” na “kujenga utamaduni na utaratibu rasmi wa kuwatambua na kuwatumia wenye vipawa vya juu” ni miongoni mwa mambo yanayoendeleza ustawi wa teknolojia ya Nano nchini Iran na kusisitiza kwamba sababu nyengine muhimu ya kudumisha maendeleo hayo ni kutoruhusu matashi ya kisiasa kuwa na ushawishi katika anga za elimu na utafiti. Ayatullah Khamenei amefafanua kuwa “kutokuwa na ghururi” na “kutotosheka na hali iliyopo pamoja na maendeleo yaliyopatikana” ni mambo mengine yatakayowezesha kusonga mbele harakati ya elimu iendayo kwa kasi na kuongeza kama ninavyomnukuu:”ni sawa, kwamba leo hii kiwango cha uwezo wa vijana wa Kiirani na kasi ya elimu ya Iran ni vya juu zaidi kulinganisha na kiwango cha wastani wa dunia; na kwa kutoa mfano, Iran iko katika nafasi ya saba duniani katika teknolojia ya Nano, lakini kutokana na kubaki nyuma nchi kwa sababu za kihistoria katika uga wa elimu, ustawi wa elimu unapasa uendelezwe kwa kasi kubwa zaidi.” Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia uadui wa madola yanayotumia mabavu dhidi ya taifa la Iran kwa sababu ya misimamo huru ya kisiasa, kijamii na kifikra ya taifa hili na kueleza kwamba uadui huo unajionyesha katika nyuga mbalimbali; kwa hivyo ili kuweza kuwa na nguvu na uwezo unaohitajika inapasa kujiimarisha zaidi siku baada ya siku. Ayatullah Khamenei leo asubuhi alitembelea maonyesho ya matunda na mafanikio yaliyopatikana katika teknolojia ya Nano, yaliyofanyika katika Husaniniya ya Imam Khomeini (MA), hapa mjini Tehran na kujionea kwa karibu juhudi na maendeleo ya kielimu ya wanasayansi na watafiti vijana wa Kiirani katika sekta za Nano na Bioteknolojia…/mh

2789402

captcha