IQNA

Rais wa Iran

Imam Khomeini aliinua bendera ya umoja baina ya Waislamu kote duniani

15:47 - October 12, 2022
Habari ID: 3475916
TEHRAN (IQNA) - Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia uwezo wa Umma wa Kiislamu katika ulimwengu wa sasa na kueleza kwamba, bendera iliyoinuliwa juu na Imamu Ruhullah Khomeini (RA) ni bendera ya umoja baina ya Waislamu kote duniani.

Rais Ebrahim Raisi wa Iran ameyasema hayo mapema leo katika ufunguzi wa Mkutano wa 36 wa Kimataifa la Umoja wa Kiislamu unaofanyika mjini Tehran.

Katika hotuba yake mbele ya hadhara kubwa ya maulamaa na wanazuoni kutoka pembe mbali mbali za dunia, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameutaja muqawama au mapambano ya Kiislamu kuwa ndiyo njia ya kuikomboa Palestina. 

Sayyid Ebrahim Raisi ameitaja kadhia ya Palestina na Quds tukufu kuwa ni suala la kwanza la Ulimwengu wa Kiislamu na kusema kuwa, njia pekee ya kuikomboa Palestina na Quds ni kusimama kidete na kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel, na hii leo inawezekana kupambana nao kwa kutegemea rasilimali nyingi zilizopo.

Akikosoa hatua ya baadhi ya nchi za Waislamu ya kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni, Raisi amesema kuwa, uhusiano kati ya serikali ni tofauti na mahusiano baina ya mataifa, na kuongeza kuwa mataifa ya eneo hili hayatakubali kuhalalishwa uhusiano baina ya serikali za nchi zao na Wazayuni maghasibu.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Marekani na utawala wa Kizayuni zinataka kuibua migawanyiko katika nchi mbalimbali, kuunda soko la silaha, kupora maslahi (mali) ya nchi mbalimbali na kuweka pembeni suala la Palestina na Quds tukufu na kueleza kuwa, Wamarekani na madola ya Ulaya ndio wavunjaji wakubwa wa haki za binadamu duniani.

Raisi amesema sera ya Iran ni kupambana na dhulma, ugaidi na makundi ya kitakfiri na kuongeza kuwa, Wamarekani wanadai kuwa wanapambana na ugaidi, lakini ni nani asiyejua kwamba shujaa wa dunia katika mapambano dhidi ya ugaidi ni Hajj Qassem Soleimani, Shahidi Abu Mahdi Al-Muhandis na Mujahidina waliolisafisha eneo hili la Magharibi mwa Asia kutokana na uwepo wa Daesh (ISIS).

Rais Ebrahim Raisi amelitaja suala la kuzidisha utambuzi na jihadi na kufafanua na kuweka wazi uhakika kuwa ni miongoni mwa majukumu ya wasomi na wanafikra wa Ulimwengu wa Kiislamu katika zama za sasa na kusema: "Hii leo suala la kubainisha na kuweka wazi haki na hakika ni wajibu wa kila mmoja wetu ili kuweka wazi nafasi ya Uislamu na Waislamu na hali ya adui na udhaifu wake kwa kutumia nyezo zote.

Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu hufanyika kila mwaka mjini Tehran kuanzia tarehe 12 hadi 17 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal kipindi cha kuadhimisha Maulidi na kuzaliwa kwa Mbora wa viumbe, Mtume Muhammad (saw).

Madhumuni ya kufanyika mkutano huo wa kimataifa wa umoja wa Kiislamu ni kujenga umoja na mshikamano baina ya Waislamu, kutayarisha mazingira ya mazungumzo na maafikiano ya wanazuoni na wanasayansi wa Kiislamu ili kukurubisha mitazamo yao ya kisayansi na kiutamaduni, kuchunguza na kuwasilisha masuluhisho ya kivitendo ili kufikia umoja wa Kiislamu na kuundwa umma mmoja katika Ulimwengu wa Kiislamu na vilevile kutatua matatizo ya Waislamu na kutoa masuluhisho yanayofaa.

4091256

captcha