IQNA

Shakhsia Katika Qur’ani /16

Ismail; Mwana wa Ibrahim na Baba wa Waarabu

22:29 - November 21, 2022
Habari ID: 3476124
TEHRAN (IQNA) – Ismail alikuwa mtoto wa kwanza wa Nabii Ibrahim –Amani ya Mwenyezi Mungu Iwe Juu Yake-(AS). Baada ya kuzaliwa, Ismail alipelekwa Makka pamoja na mama yake Hajar kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Uhamaji huu ulikuwa mwanzo wa historia iliyotangaza kuwasili kwa Uislamu.

Ismail (AS) alikuwa Nabii wa Mwenyezi Mungu ambaye kaka yake alikuwa Ishaq. Alichotetea na kufundisha Ismail (AS) kilikuwa ni sawa na mwito wa baba yake wa kuamini Mungu mmoja, ambao ulikuwa dhidi ya Shirki (ushirikina) na kuabudu masanamu.

Ismail (AS) alizaliwa wakati Ibrahim (AS) na mke wake wa kwanza Sarah walikuwa wamepoteza matumaini ya kupata watoto. Kwa pendekezo la Sarah, Ibrahim alimuoa Hajar (Hajiri) na Ismail akazaliwa.

Baadaye, Sarah pia alijifungua mtoto, Ishaq (AS), lakini aliendelea kuwaonea wivu Hajar na Ismail (AS) na akamwomba Ibrahim (AS) awafukuze. Kwa mujibu wa riwaya, Ibrahim (AS) aliwachukua Hajar na Ismail (AS) kwenda nao kwenye ardhi kame iitwayo Makka. Ibrahim (AS) aliwaacha pale na kurudi.

Ardhi hiyo ilistawi na ikatulia baada ya kisima cha Zamzam kuchipuka chini ya miguu ya Ismail (AS).

Kabila la Jarham lililokuwa likipita liliamua kusalia Makka baada ya kujua kuwa maji yamepatikana katika ardhi hiyo. Jarham lilikuwa kabila la Waarabu na Ismail alijifunza Kiarabu kutoka kwao. Kisha akaoa msichana kutoka kabila hilo.

Kwa mujibu wa riwaya za kihistoria, Ismail alikuwa na wana 12, ambao miongoni mwao Shuaib (AS) alichaguliwa kuwa Nabii wa Mwenyezi Mungu.

Ismail anajulikana kama mmoja wa mababu wa Waarabu. Amekuwa akiitwa Abu Al-Arab (baba wa Waarabu). Pia, Mtume Muhammad (SAW) alikuwa wa kabila la Kiquraishi, ambalo lilifuata asili na nasaba yake kwa Nabii Ismail (AS).

Miongoni mwa matukio muhimu wakati wa uhai wa Ismail (AS) ni kujumuika na baba yake katika kujenga Ka’aba Tukufu. Baadhi ya maelezo ya kihistoria yanasema kwamba Ka’aba ilijengwa na Nabii Adam (AS) na  kisha Ibrahim (AS) na mwanawe waliikarabati. Baada ya hapo Ibrahim (AS) na Ismail (AS) wakawa ni walinzi wa mahali hapo patakatifu.

Hadithi ya dhabihu ni hatua nyingine muhimu katika maisha ya Ismail. Katika vyanzo vingine, haswa vya Kiyahudi, ni Ishaq, mtoto mwingine wa Ibrahim, ambaye alitolewa kama dhabihu lakini kwa mujibu wa vyanzo vya Kiislamu, Mwenyezi Mungu aliamuru Ibrahimu kumchinja Ismail kwa kisu. Ismail alipojua kuhusu amri ya Mwenyezi Mungu, alikubali kutolewa kwenye njia ya Mwenyezi Mungu, Hata hivyo, Ibrahim alipoweka kisu kwenye koo la Ismail, kondoo dume alitolewa na Mwenyezi Mungu na badala yake ndiye aliyetolewa kama dhabihu.

Jina la Ismail limetajwa katika Qur’ani Tukufu mara 11, ikiwa ni pamoja na katika aya ya 85 ya Surah Al-Anbiya ambapo Ismail, pamoja na mitume wengine kama Dhu Al-Kafal na Idris, wanasifiwa kwa kuwa miongoni mwa Sabireen (wale ambao ni wenye subira).

Kulingana na riwaya, Ismail aliishi miaka 130 au zaidi. Kabla ya kifo, alikabidhi utume kwa kaka yake Ishaq. Ismail alizikwa Makka karibu na mama yake Hajar.

captcha