IQNA

Jinai ya Kigaidi

Watu 94 wauawa katika hujuma mbili za kigaidi huko Kerman Iran

21:59 - January 03, 2024
Habari ID: 3478141
IQNA-Watu wasiopungua 94 wameuawa shahidi na makumi ya wengine kujeruhiwa kufuatia mashambulio mawili ya kigiadi katika mji wa Kerman kusini mashariki mwa Iran. Taarifa zinasema yamkini idadi ya waliofariki na majeruhi ikaongezeka.

Ripoti zimebaini kuwa, milipuko miwili mikubwa imetokea leo katika mji wa Kerman kwenye njia inayoelekea katika makaburi ya mashahidi mjini Kerman.

Milipuko hiyo imetokea wakati watu walipokuwa wakielekea katika makaburi hayo ya mashahidi kwa ajili ya hauli na kumbukumbu ya mwaka wa nne wa kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, milipuko hiyo pacha imetokea jirani makaburi ya mashahidi mjini Kerman  ambapo ndipo lilipo kaburi la shahidi Qassem Soleimani.

Maafisa wa usalama wamesem tukio hilo ni hujuma ya kigaidi iliyowalenga watu wasio na hatia yoyote. Hadi sasa hakuna kundi lililotangaza kuhusika na hujuma hiyo ya kigaidi.

Kulingana na IRNA, mlipuko wa kwanza ulitokea umbali wa mita 700 kutoka kwenye kaburi la Shahidi Luteni Jenerali Soleimani na mlipuko wa pili umbali wa kilomita moja.

Shirika la habari la Tasnim lilitaja vyanzo ambavyo havikutajwa vikisema kuwa mifuko miwili iliyosheheni vilipuzi ambayo ililipuliwa kwa mbali ndiyo iliyosababisha milipuko hiyo. IRNA pia ilinukuu chanzo cha habari kikisema mifuko miwili ya mabomu iliyolipuliwa na rimoti ilisababisha milipuko hiyo.

Mlipuko wa kwanza ulitokea saa nane na dakika hamsini  kwa saa za Iran. La pili lilifanyika dakika 10 baadaye, kulingana na Meya wa Kerman Saeed Tabrizi, ISNA iliripoti.

Shirika la Hilali Nyekundu la Iran limesema waokoaji wake watatu waliuawa na mlipuko wa pili.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran Ahmad Vahidi aliuambia Mtandao wa Habari wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba jibu kali litatolewa hivi karibuni kwa wahusika.
 
Amesema mashambulizi hayo ya mabomu ni mwendelezo wa njama mbalimbali za kuua raia wasio na hatia katika mijumuiko kote nchini, nyingi zikiwa zimezuiwa na vyombo vya usalama vya Iran.
 
Alisema hali sasa iko chini ya udhibiti wa vikosi vya usalama.
Kulingana na waziri huyo, vifo vingi vilisababishwa na mlipuko wa pili. Uchunguzi wa milipuko hiyo umeanzishwa na maelezo zaidi yatatangazwa na maafisa haraka iwezekanavyo, Vahidi alibainisha.
Naye Mkuu wa Idara ya  Mahakama ya Iran Gholam-Hossein Mohseni-Ejei aliapa wahusika na waliochangia katika shambulio hilo watasakwa haraka na kufikishwa mahakamani.
 
Alilaumu mashambulizi ya magaidi wanaoungwa mkono na madola ye kibeberu ambao wana chuki kubwa dhidi ya Jenerali Soleimani, akisema wamechagua kulipiza kisasi kwa watu baada ya njama zao mbalimbali za kuikomboa nchi kuzuiwa.
 
Luteni Jenerali Soleimani, kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) na Abu Mahdi al-Muhandis, mkuu wa pili wa Kitengo cha Uhamasishaji cha Iraq (PMU) na wanajihadi wenzao waliuawa katika shambulio la ndege zisizo na rubani za jeshi la kigaidi la Marekani. Hujuma hiyo ya kigaidi iliyoidhinishwa na Rais wa wakati huo wa Merika Donald Trump ilijiri karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad mnamo Januari 3, 2020.
 
Makamanda hao wawili walikuwa wakiheshimika sana katika eneo zima la Mashariki ya Kati kwa sababu ya jukumu lao muhimu katika kupambana na kundi la kigaidi la Daesh au ISIS katika eneo hususan Iraq na Syria.

3486673

Habari zinazohusiana
captcha