IQNA

Velayati akutana na Sayyid Nasrullah, wajadili matukio ya eneo

19:27 - May 19, 2015
Habari ID: 3305555
Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya Kimataifa Ali Akbar Velayati amekutana na kiongozi wa Hizbullah ya Lebanon mjini Beirut na Rais Bashar al Assad wa Syria mjini Damascus.

Katika kikao cha Beirut siku ya Jumatatu, Sayyid Hassan Nasrallah ameipongeza Iran kwa kuendelea kuunga mkono harakati ya Hizbullah. Aidha amefafanua kuhusu matukio ya hivi karibuni katika eneo na ushindi wa Hizbullah katika vita dhidi ya Matakfiri na makundi yenye misimamo mikali. Kwa upande wake Velayati amepongeza ushindi wa harakati ya mapamabno ya Hizbullah katika vita dhidi ya Matakfiri na wenye kufurutu ada huku akisisitiza kuhusu umuhimu wa umoja wa Waislamu katika kukabiliana na makundi kama hayo. Ameongeza kuwa makundi ya Kitakfiri, yakipata himaya ya baadhi ya nchi za eneo, yanalenga kuwasilisha taswira potofu ya Uislamu na hata yanapanga kusambaratisha baadhi ya nchi za Kiislamu.
Wakati huo huo Velayati amesema mataifa ya Waislamu yanapaswa kuunganisha nguvu zao katika kupambana na adui yao mkuu wa pamoja, utawala wa Kizayuni wa Israel na wajiepushe na mifarakano.
Akizungumza katika sherehe za kufunga mkutano wa kimataifa kwenye mji mkuu wa Lebanon, Beirut jana Jumatatu, Dk. Velayati alisema kuwa, maadui wa Waislamu wanaendesha njama za kila namna za kusahaulisha kadhia ya Palestina.
Amesema, si Wapalestina peke yao walio na jukumu la kupambana vilivyo na Wazayuni, bali ni wajibu wa kila Muislamu kuendesha harakati za kuukomboa msikiti wa al Aqsa na kulinda matukufu ya Palestina.
Mshauri huyo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, suala la kurejea makwao wakimbizi wa Kipalestina haliwezi kubadilika kwani hayo ndiyo matakwa ya Wapalestina wote.
Ameongeza kuwa, mikataba yote ya kimataifa inatambua haki ya Wapalestina ya kukomboa ardhi zao kutoka katika makucha ya Wazayuni na kurejea kwenye ardhi yao.../mh

3305295

captcha