IQNA

Hujuma ya kigaidi Beirut yalaaniwa kimataifa

15:49 - November 13, 2015
Habari ID: 3447662
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani shambulio la ugaidi lililofanywa na kundi la kitakfiri la ISIS au Daesh nchini Lebanon siku ya Alhamisi ambapo watu 43 waliuawa na wengine zaidi ya 240 wamejeruhiwa.

Ban Ki-Moon amelitaja shambulio hilo kama ukatili unaochukiza na kutoa wito wa kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria waliohusika. Amekariri kuwa umoja huo utaendelea kuunga mkono serikali ya Beirut na juhudi zake za kuutokomeza ugaidi nchini humo.

Hii ni katika hali ambayo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sadiq Hussein Jaberi Ansari amelaani shambulio hilo lililoua makumi ya raia wasio na hatia na kujeruhi mamia ya wengine na kutoa mkono wa pole kwa serikali, wananchi wa Lebanon pamoja na familia za waliouawa.

Wakati huohuo harakati ya muqawama wa Lebanon Hizbullah imelaani ukatili huo na kuapa kuendeleza vita dhidi ya magaidi. Kadhalika Chuo Kikuu cha al-Azhar nchini Misri kimelaani hujuma hiyo ya kigaidi.

3447621

captcha