IQNA

Macron: Mpango wa Le Pen dhidi ya hijabu unaweza kuitumbukiza Ufaransa vita vya ndani

21:46 - April 21, 2022
Habari ID: 3475150
TEHRAN (IQNA)- Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ameonya kuwa mpango wa hasimu wake katika uchaguzi wa rais, Marine Le Pen wa kupiga marufuku hijabu katika maeneo ya umma unaweza kuibua vita ndani nchini humo.

Ametoa kauli hiyo katika mdahala wa uchaguzi wa rais uliofanyika kwa njia ya televisheni. Katika mdahalo huo, Macron amemtuhumu  Le Pen kuwa anafanya kila awezalo kuibua vita vya ndani nchini Ufaransa kwa kusema: "Le Pen anajaribu kuitumbukiza Ufaransa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa kuzingatia matamshi aliyoyatoa mgombea huyo wa mrengo wa kulia ambaye alitangaza rasmi kuwa, kama atachaguliwa kuwa Rais wa Ufaransa atapiga marufuku vazi la hijabu katika maeneo ya umma."

Mgombea huyo wa kiti cha rais nchini Ufaransa kwa tiketi ya chama cha National Rally, amesisitiza kuwa anafanya hilo ili eti kwa ajili ya kuheshimu usawa wa wanawake na wanaume na kwamba anaamini kuvaliwa vazi hilo la Kiislamu katika maeneo ya umma kunakiuka msingi huo.  

Macron amemwambia Marine Le Pen kwamba: "Kile unachokipendekeza ni kusaliti ari ya Ufaransa na hatua yako hii ni sawa na kuwafukuza katika maeneo ya umma mamilioni ya raia wenzetu wa Kiislamu."  

Hivi karibuni mgombea huyo wa kiti cha urais wa Ufaransa kwa tikiti ya chama chenye siasa kali cha mrengo wa kulia, Marine Le Pen, alitamka wazi kuwa iwapo atashinda kiti cha urais, atapiga marufuku kuchinja wanyama kwa njia ya Kiislamu ya Kiyahudi, na vilevile vazi la staha la mwanamke wa Kiislamu, hijabu.

Le Pen alidai kuwa atafanya hivyo ili kujibu matakwa ya Wafaransa waliowengi. Hata hivyo duru mbalimbali za habari zinasema, uamuzi huo unatokana na sera na mitazamo ya chuki na ubaguzi ya mwanasiasa huyo wa Ufaransa dhidi ya Uislamu na wahajiri.  

Duru ya pili ya uchaguzi wa rais wa Ufaransa imepangwa kufanyika tarehe 24 mwezi huu; ambapo washindi wa duru ya kwanza yaani Macron na Le Pen watachuana katika uchaguzi huo. 

3478591

captcha